Hazina-Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar

Msajili wa Hazina Zanzibar Aongoza Kikao Kazi na Ziara ya Ukaguzi wa Mali Kisiwani Pemba

September 12, 2025

Msajili wa Hazina Zanzibar, Ndugu Waheed Muhammad Ibrahim Sanya, ameongoza kikao kazi na wafanyakazi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina – Pemba, kikao kilicholenga kuimarisha utendaji kazi bora, wenye tija na ufanisi katika taasisi hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho, Ndugu Sanya aliwahimiza watumishi kuendelea kujenga mshikamano, nidhamu na ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Amesisitiza kuwa jukumu la Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kuhakikisha mashirika ya umma yanaendeshwa kwa ufanisi na kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Zanzibar.

Aidha, amewataka watumishi kuongeza bidii katika kuwahudumia wananchi kwa weledi na uwajibikaji, ili kuimarisha imani ya umma kwa mashirika ya umma na taasisi zinazoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Pamoja na hayo, Ndugu Sanya aliwahimiza wafanyakazi kutunza amani na utulivu katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2025, sambamba na kushiriki kikamilifu katika zoezi la upigaji kura, ili kuendelea kuimarisha demokrasia na mshikamano wa kitaifa.

Katika ziara yake kisiwani Pemba, Msajili wa Hazina Zanzibar pia alitembelea Msitu wa Ngezi, ambapo alikagua mali za serikali zilizopo eneo hilo, na kuangalia mali zinazotakiwa kuondoshwa ili kupisha ujenzi wa barabara. Ziara hiyo imelenga kuhakikisha rasilimali za serikali zinasimamiwa ipasavyo sambamba na kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kikao kazi na ziara hiyo vimekuwa fursa muhimu kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar kuimarisha ufanisi wa utendaji wake, sambamba na kuweka mikakati madhubuti ya kulinda na kusimamia mali za serikali kwa manufaa ya taifa.