Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar imefanya ziara ya kikazi katika Chuo kikuu cha Ardhi Dar es Salaam kwa lengo la kujenga na kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma unaolenga kukuza ujuzi na weledi kwa wasimamizi wa mali za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Ziara hiyo imelenga kubadilishana uzoefu na maarifa katika masuala ya usimamizi wa mali, tathmini ya ardhi na majengo, pamoja na matumizi ya mbinu za kisasa katika upangaji na uendelezaji wa rasilimali za umma.
Akizungumza katika ziara hiyo Msajili wa Hazina Zanzibar Waheed Muhammad Ibrahim Sanya, alisema Ofisi yake inalenga kuwajengea uwezo watumishi wake ili waweze kusimamia mali za umma kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia misingi ya kitaaluma.

Aidha alisema Chuo cha Ardhi Dar es Salaam kina utaalamu na uzoefu mkubwa katika kutoa mafunzo ya kitaaluma yanayohusiana na usimamizi wa ardhi na mali, hivyo ni mshirika muhimu katika jitihada za serikali za kuboresha utendaji wa taasisi zake.
Alisema mafunzo hayo yatachangia kuongeza tija, kudhibiti upotevu wa mali za umma na kuongeza mapato yatokanayo na mali za serikali.
Waheed alibainisha kwamba ofisi yake ina jukumu la kusimamia mashirika ya umma ya serikali pamoja na mali zote zinazomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Alisema licha ya uwepo wa mali hizo na mifumo ya usimamizi, bado kiwango cha ufanisi na uwezo wa rasilimali watu (capacity) katika usimamizi wa mali kipo chini ikilinganishwa na Tanzania Bara.
Alibainisha kuwa watu wengi hawafahamu dhana ya mali hivyo wameona kukaa na chuo ili kushirikiana kuwapa taaluma kwa lengo la kuwajenga wakuu wa vitengo kujua umuhimu wa mali.
“Changamoto kubwa iliyopo ni uelewa mdogo wa dhana ya mali za umma miongoni mwa watendaji wengi wa serikal kutokana na hali hiyo, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeona umuhimu wa kushirikiana na taasisi za elimu ya juu, hususan Chuo cha Ardhi, ili kuwajengea uwezo wakuu wa vitengo na wasimamizi wa mali kuhusu umuhimu, thamani na mbinu bora za usimamizi wa mali za umma,” alisema
Aidha, Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar itaandaa miongozo na sera zitakazowawezesha watumishi hao kujiendeleza kitaaluma na kuendana na viwango vya kitaifa na kimataifa vya usimamizi wa mali.

Sambamba na hilo, ofisi hiyo imepanga kuandaa majukwaa (forum) yatakayozikutanisha vyuo vikuu vya Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma na kuweka mkakati wa pamoja wa kukuza taaluma ya usimamizi wa mali.
“Hatua hii inalenga kupata njia shirikishi zitakazosaidia kufikia lengo la kudhibiti, kulinda na kuongeza tija ya mali za umma kwa manufaa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Zanzibar na Taifa kwa ujumla,” alisema.
Alisema ni matumaini yake kuwa watashirikiana pamoja ili kutoa programu za mafunzo na masomo ya kujiendeleza kitaaluma ili kuwawezesha watumishi wa serikali watapatiwa fursa ya kuongeza ujuzi wao katika maeneo ya tathmini, uendelezaji na udhibiti wa mali.
“Lengo letu ni kuhakikisha kitengo cha mali Zanzibar kinasimamiwa vizuri na kufikia lengo lilokusudiwa la kuanzishwa kwake katika kutunza mali,” alibainisha.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo hicho Professa Evarist Liwa, alisema chuo kina historia ndefu na mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya ardhi na taaluma kwani awali Tanzania ilikuwa ikipeleka wataalamu wa upimaji ardhi kwenda kufundisha katika nchi jirani ikiwemo Nairobi, hali inayoonesha uwezo na ubora wa kitaaluma uliokuwepo tangu miaka ya nyuma.
Alifafanua kuwa tangu mwaka 1996 na baadae mwaka 2017, Chuo cha Ardhi kimepanua wigo wa taaluma zake kwa kiasi kikubwa, kutoka kuzingatia masuala ya ardhi pekee hadi kutoa programu mbalimbali za kisasa zinazokidhi mahitaji ya maendeleo ya nchi.
Miongoni mwa programu hizo alisema ni pamoja na Usimamizi wa Mifumo ya Taarifa (Information Systems Management), Uhandisi wa Ujenzi (Civil Engineering) pamoja na taaluma nyingine mbalimbali zinazolenga kukuza ujuzi na weledi wa wataalamu katika sekta za ardhi, miundombinu na usimamizi wa rasilimali za umma na taaluma nyingine zinazochangia uzalishaji wa wataalamu wenye ujuzi mpana na unaohitajika katika soko la ajira.

Alisema kupitia programu hizo, wanafunzi wengi wamepata maarifa na ujuzi unaowawezesha kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Hata hivyo, akibainisha kuwa chuo kimekuwa mshirika muhimu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani kimeshiriki katika kuandaa mipango miji (master plans) ya majengo na maeneo mbalimbali ya serikali, hatua iliyochangia kuboresha upangaji na uendelezaji wa miundombinu ya umma.
Sambamba na hayo, alisema chuo kimekuwa kikishirikiana na mihimili mbalimbali ya serikali kwa kupokea na kutoa mafunzo kwa kamati za Baraza la Wawakilishi, ikiwemo Kamati ya Fedha, ili kuwawezesha kupata uelewa mpana wa masuala ya ardhi na mali za umma.
Alifafanua kuwa chuo kina programu maalumu za usimamizi wa mali za umma ikiwemo Land Management na programu nyingine zinazowaandaa wataalamu kuelewa hali, thamani na matumizi ya mali za taifa kabla ya kushiriki katika usimamizi wake.
Alisema dhamira ya chuo ni kushiriki kikamilifu katika kujenga taifa kwa kuzalisha wataalamu na kuhakikisha kazi wanayoifanya inaacha alama ya kudumu katika maendeleo ya nchi.
Alifahamisha kuwa chuo pia kinatoa Programu ya Usimamizi wa Majengo na Miundombinu (Facility Management) na hupeleka wanafunzi katika maeneo mbalimbali kwa mafunzo ya vitendo, hatua inayowaandaa kukabiliana na changamoto halisi za usimamizi wa majengo na miundombinu.
Alisisitiza kuwa chuo kipo tayari kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar katika maeneo mbalimbali ya kitaaluma na kiutendaji kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.
“Chuo chetu kipo tayari kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia programu za mafunzo, tafiti za pamoja na ushauri wa kitaaluma kwani tunaamini ushirikiano huu utakuwa chachu ya kuboresha mfumo wa usimamizi wa mali Zanzibar na kuendana na mahitaji ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi,” alisema


