Hazina-Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar

Ofisi ya Msajili wa Hazina yaingia Mashirikiano na chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT)

January 19, 2026

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar, imeandaa mpango maalumu wa usimamizi wa mali za umma kwa lengo la kuhakikisha mali zote za serikali zinasimamiwa kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji.

Akizungumza katika kikao maalum cha mashirikiano na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji Dar es salam, Msajili wa Hazina Zanzibar Waheed Muhammad Sanya, alisema mpango huo unalenga kulinda thamani ya mali za umma, kuongeza tija katika matumizi yake pamoja na kuzuia upotevu unaoweza kujitokeza kutokana na usimamizi usiozingatia taratibu.

Alisema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuimarisha mifumo ya usimamizi wa rasilimali za umma, ili ziweze kuchangia kikamilifu maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya wananchi.

Alisema mali za serikali zipo lakini usimamizi wake umekuwq wa kawaida lakini pamoja na mifumo lakini uwezo wake upo chini katika kusimamia mali za umma ukilinganisha na Tanzania bara

Aidha Waheed alibainisha kwamba watu wengi hawafahami dhana ya mali hivyo wameona ipo haja ya kukaa na chuo hicho ili kushirikiana kuwapa taaluma ili kuwajengea uwezo wakuu wa vitengo kujua umuhimu wa mali.

Alisema mpango huo umejikita katika kuweka mifumo madhubuti ya utambuzi, usajili, tathmini na ufuatiliaji wa mali zote zinazomilikiwa na taasisi za serikali.

Hata hivyo, alisema kupitia mpango huo, taasisi za umma zitatakiwa kuzingatia kanuni na miongozo iliyowekwa katika matumizi, matengenezo na uendelezaji wa mali za serikali, huku taarifa za mali hizo zikiwekwa katika mifumo ya kidijitali ili kurahisisha ufuatiliaji na kufanya maamuzi sahihi. Hatua hiyo inatarajiwa kusaidia kuongeza uwazi, kupunguza mianya ya ubadhirifu na kuimarisha uwajibikaji kwa viongozi na watendaji wa umma.

Alisema utekelezaji wa mpango huo utahusisha ushirikiano wa karibu kati ya wizara, idara na taasisi za serikali pamoja na wadau wengine muhimu, ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.

Hivyo alisema ni imani yake mpango huo unatakuwa chachu ya kuboresha usimamizi wa mali za umma na kuongeza mchango wake katika kukuza uchumi wa Zanzibar na ustawi wa wananchi.

Akizungumzia ushirikiano kati ya ofisi yake na Chuo Kikuu cha Ardhi, alisema anaamini watendaji wa taasisi za serikali watapata maarifa na suluhisho bunifu yatakayosaidia kuboresha usimamizi wa mali za umma kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji na uendelevu.

Alisema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuimarisha mshikamano kati ya taasisi za elimu ya juu na taasisi za umma katika kufanikisha malengo ya serikali ya kutunza mali za umma.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo hicho Professa Evaristo Liwa, alisema wapo tayari kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina katika nyanja mbalimbali zitakazochangia kuimarisha usimamizi wa rasilimali na mali za umma kwa manufaa ya maendeleo ya taifa.

Alisema watatumia utaalamu walionao wa kitaaluma, tafiti na ubunifu kusaidia juhudi za serikali katika kusimamia mali za umma kwa ufanisi, uwazi na tija.

Aliiomba Ofisi ya Msajili wa Hazina kuharakakisha kusaini mashirikiano hayo haraka ili waweze kufanikisha lengo la utoaji wa elimu ambayo itasaidia watendaji wa taasisi za serikali kusimamia ipasavyo mali za umma.