Serikali Yasisitiza Umuhimu wa Gawio la Mashirika ya Umma
Zanzibar – Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kuchukua jitihada mbalimbali kuhakikisha Taasisi na Mashirika ya Umma yanafanya vizuri katika ugawaji wa gawio ili kuchochea maendeleo ya nchi.

Akizungumza katika hafla ya uwasilishaji wa Ripoti ya Tathmini ya Mikataba ya Kiutendaji kwa mwaka 2024/2025, iliyofanyika katika ukumbi wa ZURA, Maisara, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dkt. Juma Malik Akil, alisema bado kuna baadhi ya Taasisi hazijafanya vizuri katika kugawa gawio, jambo linalochelewesha juhudi za Serikali katika kukuza uchumi.

Aidha, aliipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa usimamizi wake madhubuti, pamoja na kupongeza Mashirika ya Umma kwa utendaji wao unaochangia ukuaji wa uchumi wa Taifa. Hata hivyo, alisisitiza kuwa bado changamoto kubwa ipo kwenye eneo la gawio, kwani upatikanaji wa gawio bado hauridhishi. Alifafanua kuwa gawio kutoka Taasisi na Mashirika ya Umma lina mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo miradi mikubwa inayotekelezwa kutokana na akiba ya Serikali kupitia mapato ya ndani. Vilevile alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuchukua juhudi za kuelimisha Taasisi juu ya nafasi na jukumu la Ofisi ya Msajili wa Hazina katika kusimamia mashirika hayo.

Kwa upande wake, Msajili wa Hazina Zanzibar, Ndg. Wahid Ibrahim Sanya, alisema ofisi yake ina jukumu la kusaini mikataba mbalimbali na Taasisi za Umma, ambayo hupaswa kuwasilishwa kwa ripoti za utekelezaji ili kufanyiwa tathmini. Aliongeza kuwa changamoto kubwa bado ni uelewa mdogo wa baadhi ya Taasisi kuhusu utekelezaji wa majukumu yao ya kisheria na kiutendaji.

Akiwasilisha ripoti ya tathmini ya mwaka 2024/2025, Mkuu wa Idara ya Mitaji ya Umma na Uwekezaji, Ndg. Ramia Mohammed Ramia, alisema Mashirika ya Umma yameonyesha maendeleo katika maeneo mbalimbali:

- Utawala bora na udhibiti: 84.7%
- Usimamizi wa wafanyakazi: 68.08%
- Utekelezaji wa majukumu ya kimsingi: 74.8%
- Huduma kwa wateja: 73.6%
- Usimamizi wa fedha: 67.36%
Hata hivyo, ripoti imebainisha changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa mafunzo ya mara kwa mara, udhaifu katika ukusanyaji wa mapato na gharama kubwa za uendeshaji.