Hazina-Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma akabidhi Muundo wa Utumishi kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar

September 11, 2025

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma Zanzibar, Bwana Kubingwa Mashaka Simba, amesisitiza umuhimu wa kutumia muundo wa utumishi ipasavyo katika kuboresha maslahi ya watumishi wa umma. Kauli hiyo aliitoa katika hafla ya kukabidhi muundo wa utumishi kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar.

Akizungumza katika hafla hiyo, Ndugu Simba alisema kuwa muundo wa utumishi ni nyenzo muhimu ya kuimarisha haki na maslahi ya watumishi, hivyo haupaswi kuwekwa kwenye makabati bali unapaswa kufanyiwa kazi kwa vitendo.

Alisisitiza kuwa ni jukumu la watendaji kuhakikisha watumishi wanapatiwa elimu kuhusu utekelezaji wa majukumu yao kwa mujibu wa muundo huo, jambo ambalo litasaidia kuongeza ufanisi na uwajibikaji.

Aidha, alieleza kuwa upimaji wa watumishi na upandishaji wa madaraja unatakiwa kufanyika kwa haki, kwa kuzingatia sifa na utendaji wa kila mmoja. “Watumishi lazima wapimwe na kupandishwa madaraja kwa mujibu wa stahiki zao, na ni wale wanaostahili pekee ndio watakaopata fursa hiyo,” alisema.

Katibu Mtendaji huyo pia alihimiza watendaji wa taasisi kujua na kuelewa vizuri scheme of service, akibainisha kuwa Kamisheni ipo tayari kutoa ushirikiano na elimu kuhusu muundo uliopitishwa, ili kuhakikisha unatekelezwa kwa ufanisi na kwa manufaa ya watumishi pamoja na taasisi kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali watu, Utawala na Mipango wa Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar, Bwana Makunga Ali Mzee alisema, kupitishwa kwa muundo huo kutapelekea wafanyakazi kutimiza majukumu yao inavyotakiwa, hali ambayo itapelekea ufanisi katika taasisi. Aidha kwa upande mwengine ameishukuru kamisheni kwa kukamilisha na kukabidhi muundo huo kwa wakati.