Hazina-Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar

NAIBU GAVANA MSTAAFU WA BENKI KUU YA TANZANIA (BOT) AELEZEA KUHUSU UMUHIMU WA USIMAMIZI WA MASHIRIKA YA UMMA

October 7, 2025

Naibu Gavana Mstaafu wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Bw. Juma Hassan Reli, akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Wiki ya Mashirika ya Umma Zanzibar inayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 11 hadi 15 Oktoba 2025 katika Viwanja vya Mapinduzi Square, Kisonge, ameeleza kuwa serikali inawekeza kwenye mashirika ya umma kwa madhumuni ya kupata mapato kupitia gawio na kodi.

Amefafanua kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar imeanzishwa kwa lengo la kutekeleza malengo ya Serikali Kuu kwa kuhakikisha mashirika ya umma yanaendeshwa kwa ufanisi, uwazi, na tija.

Bw. Reli amesema:

“Ofisi ya Msajili wa Hazina inapaswa kuandaa mikataba kwa mashirika yote, na mashirika hayo ni lazima yafuate masharti ya mikataba hiyo ili kupimwa mwenendo na ufanisi wake.”

Ameongeza kuwa jukumu la ofisi hiyo linahusisha:

  • Kufuatilia mahesabu ya kila shirika
  • Kuweka utaratibu wa kupima ufanisi wa bodi za wakurugenzi
  • Kuhakikisha bodi zinaundwa na wajumbe wenye taaluma mbalimbali
  • Kutathmini kama shirika linafaa kuendelea au kufutwa

Aidha, ametoa wito kwa mashirika yasiyoleta faida kufanyiwa utafiti wa kina ili kubaini chanzo cha changamoto na kuweka mikakati sahihi ya maboresho.

Mwisho, amesisitiza kuwa mashirika ya umma yanapaswa kuendeleza utamaduni wa kibiashara (corporate culture) ili kuongeza tija na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.