Hazina-Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar

Msajili wa Hazina Zanzibar Aongoza Kikao Kazi na Ziara ya Ukaguzi wa Mali Kisiwani Pemba

Msajili wa Hazina Zanzibar, Ndugu Waheed Muhammad Ibrahim Sanya, ameongoza kikao kazi na wafanyakazi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina – Pemba, kikao kilicholenga kuimarisha utendaji kazi bora, wenye tija na ufanisi katika taasisi hiyo. Akizungumza katika kikao hicho, Ndugu Sanya aliwahimiza watumishi kuendelea kujenga mshikamano, nidhamu na ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Amesisitiza kuwa jukumu la Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kuhakikisha mashirika ya umma yanaendeshwa kwa ufanisi na kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Zanzibar. Aidha, amewataka watumishi kuongeza bidii katika kuwahudumia wananchi kwa weledi na uwajibikaji, ili kuimarisha imani ya umma kwa mashirika ya umma na taasisi zinazoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina. Pamoja na hayo, Ndugu Sanya aliwahimiza wafanyakazi kutunza amani na utulivu katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2025, sambamba na kushiriki kikamilifu katika zoezi la upigaji kura, ili kuendelea kuimarisha demokrasia na mshikamano wa kitaifa. Katika ziara yake kisiwani Pemba, Msajili wa Hazina Zanzibar pia alitembelea Msitu wa Ngezi, ambapo alikagua mali za serikali zilizopo eneo hilo, na kuangalia mali zinazotakiwa kuondoshwa ili kupisha ujenzi wa barabara. Ziara hiyo imelenga kuhakikisha rasilimali za serikali zinasimamiwa ipasavyo sambamba na kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kikao kazi na ziara hiyo vimekuwa fursa muhimu kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar kuimarisha ufanisi wa utendaji wake, sambamba na kuweka mikakati madhubuti ya kulinda na kusimamia mali za serikali kwa manufaa ya taifa.

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma akabidhi Muundo wa Utumishi kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma Zanzibar, Bwana Kubingwa Mashaka Simba, amesisitiza umuhimu wa kutumia muundo wa utumishi ipasavyo katika kuboresha maslahi ya watumishi wa umma. Kauli hiyo aliitoa katika hafla ya kukabidhi muundo wa utumishi kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar. Akizungumza katika hafla hiyo, Ndugu Simba alisema kuwa muundo wa utumishi ni nyenzo muhimu ya kuimarisha haki na maslahi ya watumishi, hivyo haupaswi kuwekwa kwenye makabati bali unapaswa kufanyiwa kazi kwa vitendo. Alisisitiza kuwa ni jukumu la watendaji kuhakikisha watumishi wanapatiwa elimu kuhusu utekelezaji wa majukumu yao kwa mujibu wa muundo huo, jambo ambalo litasaidia kuongeza ufanisi na uwajibikaji. Aidha, alieleza kuwa upimaji wa watumishi na upandishaji wa madaraja unatakiwa kufanyika kwa haki, kwa kuzingatia sifa na utendaji wa kila mmoja. “Watumishi lazima wapimwe na kupandishwa madaraja kwa mujibu wa stahiki zao, na ni wale wanaostahili pekee ndio watakaopata fursa hiyo,” alisema. Katibu Mtendaji huyo pia alihimiza watendaji wa taasisi kujua na kuelewa vizuri scheme of service, akibainisha kuwa Kamisheni ipo tayari kutoa ushirikiano na elimu kuhusu muundo uliopitishwa, ili kuhakikisha unatekelezwa kwa ufanisi na kwa manufaa ya watumishi pamoja na taasisi kwa ujumla. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali watu, Utawala na Mipango wa Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar, Bwana Makunga Ali Mzee alisema, kupitishwa kwa muundo huo kutapelekea wafanyakazi kutimiza majukumu yao inavyotakiwa, hali ambayo itapelekea ufanisi katika taasisi. Aidha kwa upande mwengine ameishukuru kamisheni kwa kukamilisha na kukabidhi muundo huo kwa wakati.